Rais Samia aiagiza TRC kufunganisha reli na usafiri wa anga
Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuhakikisha vipande vya reli ya kisasa ya SGR inayoendelea kujengwa nchini vinakamilika kwa wakati na kwa viwango na ubora uliokubaliwa.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa huduma za Usafiri wa Treni ya Kisasa (SGR) kuanzia eneo la Kilometa 0 Stesheni Jijini Dar es Salaam- Morogoro hadi Dodoma leo, amesema tayari Serikali ina mipango ya kuambatanisha reli ya hiyo na maeneo mengine.
Rais Samia pia ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa meli za kubeba mizigo unaoendelea kwenye maziwa mbalimbali unakamilika kabla ya mradi wa SGR haujaisha ili reli isomane kibiashara na bandari za Bahari na maziwa makuu.
“Ninawataka pia muhakikishe tunafunganisha reli na usafiri wa anga ikiwemo kuingiza reli katika Terminal 3 ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ambao nimefahamishwa ni urefu wa takribani 0.6 kilometa, kilomita moja kidogo tu najua mnaweza, ingizeni kule ile ili mizigo itoke moja kwa moja na iingie kwenye reli,” amesema.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha inatumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA kuendesha mradi huo wa reli ya SGR ikiwemo mifumo ya ulinzi wa reli, ukataji tiketi nakadhalika.
“Tusingependa kusikia tunarudi tena kwenye tiketi za mkono, hakikisheni mifumo yenu inalindwa ili isiweze kuingiliwa na wale wasiotutakia mema,” amesisitiza.
Mbali na hayo ametoa rai kwa TRC kuwa makini zaidi kuhusu usalama wa abiria na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa za kiwango pamoja na kuweka mifumo thabiti ya matengenezo.