Rais Samia Suluhu Hassan amesema Septemba mwaka huu, Mkoa wa Katavi utaanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa na kuachana na umeme wa jenereta ambao unagharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya shilingi bilioni 2 kila mwezi.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Inyonga mkoani Katavi, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani humo, baada ya kukagua Kituo cha Kupoza Umeme wa Gridi ya Taifa.
Rais Samia ametoa wito kwa wananchi wa Katavi kutunza mradi huo ambao ujenzi wa kituo umegharimu shilingi bilioni 48 na shilingi bilioni 116 kujenga njia za usambazaji na kupokea umeme huku akiwasihi kutumia umeme huo kwa maslahi ya kiuchumi.
“Umeme huu pia utakuza uwekezaji ndani ya mkoa wetu, ndani ya wilaya yetu hii. Pakiwa na umeme wa uhakika, haukatiki, wawekezaji bila shaka watakuja na shughuli za uwekezaji zitaendelea vyema,” amesema.
Ameongeza kuwa “umeme huo utakapokuja kutumiwa ulipwe kama mtu anavyotumia. Umeme si huduma ni biashara, ni huduma kwamba inakupa uwezo kutumia na kuutumia kiuchumi, na kwa maana hiyo lazima tulipe umeme ili umeme uendelee kuwaka.”
Aidha, amewapongeza baadhi ya wananchi wa mkoa huo waliokubali mradi wa umeme upite kwanza na fidia ifuate baadaye, akiwahakikishia kuwa serikali italipa fidia yote.
Rais Samia pia amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujipanga vyema katika shughuli ya usambazaji na uunganishaji wa umeme kwenye taasisi na majumbani baada ya kazi ya kuingiza umeme kwenye gridi kumalizika.