Rais Samia aipa milioni 10 familia iliyopoteza watoto wanne kwenye ajali

0
59

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 10 kama mkono wa pole kwa familia ya Mzee Hashim Msuya iliyofikwa na msiba wa kupoteza watoto wanne kufuatia ajali iliyotokea eneo la Mbwewe, Pwani Agosti 3, 2023.

Akiwasilisha salamu za pole za Rais, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amefika nyumbani kwa mzee Msuya Mbezi Beach Kinondoni mkoani Dar es Salaam na kukabidhi ubani huo pamoja na mahitaji mengine kama sukari, mchele, ngano, mafuta ya kupikia, chumvi, maziwa na vinywaji mbalimbali kama maji, soda na yogati, vilevile vitambaa na vitenge kwa ajili ya kuwafariji wafiwa hao.

Aidha, Chalamila amesema msisitizo wa Rais ni kuwa wazazi hao ambao ni wazee waliofikwa na msiba huo kupatiwa matibabu bila malipo katika Hospital ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na hata Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma wakati wote watakapo hitaji huduma za afya.

Sambamba na hilo, RC Chalamila amesema Rais Samia ameiomba familia hiyo kuendelea kuwasimamia watoto waliopoteza wazazi wao ili wafikie ndoto zao.

Mzee Msuya amemshukuru Rais kwa upendo wake wa kuwafariji katika kipindi hicho na kumtakia kheri katika majukumu yake ya kuiongoza nchi.

“Mimi Msuya ni nani hadi mkuu wa nchi aje kunifariji, mwenyezi Mungu ambariki sana Rais Dkt Samia,” amesema.

Send this to a friend