Rais Samia aipa Taifa Stars milioni 500 kwa kufuzu AFCON

0
43

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 500 kwa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) baada ya kufukuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 nchini Ivory Coast.

Akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu ambaye aliongoza msafara wa timu hiyo nchini Algeria, amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya hadi dakika ya mwisho kufuzu kwa suluhu katika mchezo wa mwisho wa Kundi F nchini humo.

“Mtakumbuka wakati wa kujiandaa na mechi ya Uganda kule nyumbani Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 500, timu ikifuzu. Nafurahi kuwaambia kwamba hizo fedha sio tu kwamba zitatolewa, zimekwisha letwa wizarani kwa ajili yenu” amesema Yakubu.

Taifa Stars ikiwa na alama 8 imeungana na Algeria yenye alama 16 katika kundi hilo kushiriki mashindano ya AFCON yatakayofanyika Ivory Coast na kuziacha nje ya mashindano hayo timu za Uganda waliomaliaza na alama 7 na Niger waliomaliza na alama 2 huku Tanzania ikishiriki mashindano ya AFCON kwa mara ya tatu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri.

Send this to a friend