Rais Samia aipongeza Tembo Warriors, atoa maagizo TFF na wizara

0
50

Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wenye Ulemavu, Tembo Warriors, kwa kufanikiwa kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Uturuki mwaka 2022.

Timu hiyo imefikia hatua hiyo baada ya kuifunga timu ya Cameroon jumla ya magoli 5-0 na kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya wenye ulemavu Afrika (CANAF) yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.

“Naipongeza Timu ya Taifa ya Walemavu ya Mpira wa Miguu (Tembo Warriors) kwa kufuzu Kombe la Dunia nchini Uturuki Oktoba, 2022,” ameandika Rais kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aidha amewataka viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufanya maandalizi mazuri zaidi kuelekea michuano hiyo ili timu iwe bora na iitangaze vyema Taifa.

Ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri, Rais Samia alitoa TZS milioni 150 kwa ajili ya maandalizi ambazo zilikabidhiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea timu hiyo kuona ilivyojiandaa.

Kwa upande wake Rais wa TFF, Wallace Karia amesema mafanikio ya timu hiyo yawe chachu kwa timu nyingine zinazoliwakilisha Taifa kimataifa kufanya vizuri.

Mashindano hayo yamegharamiwa na wizara ambapo yanafanyika nchini kwa mara ya kwanza.

Send this to a friend