Rais Samia airuhusu NHC ikope ikamilishe miradi ya Kawe na Morocco Square

0
45

Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukopa TZS bilioni 173.9 kwa ajili ya kukamilisha miradi ilyokwama kwa miaka minne ikiwa ni pamoja na Kawe 711, Morocco Square na Kiwanja 300 Regent Estate.

Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba 1,000 zinazojengwa na NHC jijini hapo na kusema kuwa wanunuzi wa nyumba za Iyumbu zinazojengwa na NHC watanunua nyumba kwa riba ya 9% kwa kuwa Benki ya Azania imekubali kuwakopesha kwa riba nafuu.

Dk. Kijazi alifafanua kuwa Serikali ililipatia shirika mkopo nafuu wa TZS bilioni 20 wenye riba ya 6.75% ambazo zilitolewa kupitia benki ya Azania ambazo zitatumika kama mtaji.

“Mkopo huu ni wa miaka 15 ambao utalipwa kwa muda wa miaka 12 baada ya miaka mitatu ya kipindi cha ujenzi wa mradi wa nyumba hizo, na lengo la kutoa mkopo ni kuiwezesha NHC kujenga nyumba ili kusaidia upatikanaji wa makazi hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma,” amesema Dk Kijazi.

Ameongeza kuwa ili kufikia nyumba hizo 1,000 ambazo zitagharimu takribani TZS bilioni 71 hadi kukamilika, NHC itaendelea kujenga nyumba za awamu ya pilli na ya tatu kwa kutumia pesa zinazopatikana baada ya nyumba kuuzwa.

Awamu ya kwanza ya mradi ilihusisha ujenzi wa nyumba 404 uliogharimu TZS biloni 21.4 na unatarajia kukamilika hivi karibuni huku nyumba zinazojengwa Chamwino kupangishwa na nyumba 303 zinazojengwa Iyumbu kuuzwa kwa wananchi wanaozihitaji.

Hata hivyo alieleza kuwa utekelezaji unafanyika kwa kuwatumia wataalamu wa ndani na pia utekelezaji huo unaenda vizuri na umewezesha upatikanaji wa ajira za moja kwa moja 600 kwa siku.

Send this to a friend