Rais Samia aitaka Posta iendane na wakati na mahitaji ya soko

0
39

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na maendelo ya mwanadamu yanavyozidi kushika kasi, mfumo wa posta nao hauwezi kubaki kama ulivyokuwa katika miaka iliyopita, lazima ubadilike kuendana na wakati na mahitaji ya soko kama lilivyo ili kujenga umuhimu wa uwepo wa posta.

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha ambapo ameeleza kuwa amefarijika kuona umoja huo unatambua vyema mwelekeo mpya wa shughuli za posta na hivyo bila shaka wamejizatiti kwenda kidijitali.

“Maazimio yaliyofikiwa kuhusu mikakati mbalimbali ya kuleta mabadiliko katika biashara na shughuli za posta, yaende kuakisi wakati tulionao na mahitaji ya ulimwengu wasasa tulionao,” amesema Rais.

Aidha, amependekeza kuwa posta za Afrika ziwe na mfumo mmoja utakaowezesha kufanyika kwa biashara mtandao kwakuwa tayari takribani kila posta imeanzisha maduka mtandao ili kuwarahisishia wafanyabiashara shughuli zao.

Rais Samia awataka viongozi kutotumia vyeo kunyanyasa watu

Mbali na hayo, amewaomba wanachama wengine wa Umoja wa Afrika ambao hawajajiunga na umoja huo wafanye hivyo na wale ambao wana malimbikizo ya michango watekeleze wajibu wao.

“Nimetaarifiwa kwamba ni nchi 45 tu ndio zimejiunga na nimeonyeshwa wakati natembelea jengo, na kati ya hizo, nyingine bado ziko nyuma sana katika kulipa ada zao kwa karibu miaka mingi tu zaidi ya 30.

“Nadhani hawa ndio wale waliopoteza matumaini na system hizi za posta lakini kwa kuwepo jengo hili na maendeleo yanayotokea, tukiweza kuwaonesha wenzetu na wenyewe watapata matumaini na kurudi kuwa wanchama ili wote twende pamoja,” ameeleza.

Ahadi ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya PAPU ilitolewa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1980 baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa makao makuu ya umoja huo.

Send this to a friend