Rais Samia aitaka Serikali kuongeza uwezo wa kukabiliana na maafa
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha inaongeza uwezo na utaalam wa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea nchini ikiwemo kuwa na vifaa mbalimbali vya uokozi ili kuepusha athari kubwa zaidi pamoja kuimarisha uwezo wa kuweza kubaini mapema viashiria au hatari zinazojitokeza.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Hanang mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko pamoja na kuwapa pole waathirika wa maafa hayo.
“Jingine kwa Serikali ni kwamba, tuhakikishe kwamba tunaongeza uwezo wetu katika kukabiliana na maafa wa vifaa lakini pia utaalam katika kukabiliana na maafa ya namna hii. Na nashukuru katika janga hili, serikali bado hatukupata msaada kutoka nje, tumeweza kufanya wenyewe yote na yote yanakwenda vizuri,” amesema.
Aidha, ameelekeza kufanyike uchunguzi wa taarifa za kina wa athari zilizojitokeza ikiwemo mali zilizopotea watu walioathirika pamoja na eneo ambalo Serikali inaweza kuwahamishia waathirika wa maporomoko hayo, amabapo eneo hilo tayari limepatikana.
Mbali na hilo amewataka wanakamati wanaohudumia waathirika kufanya matumizi mazuri ya fedha zinazokusanywa huku akieleza kuwa fedha hizo zitumike kufanya marekebisho na kuwafariji waliofikwa na janga hilo na si kumnufaisha mtu binafsi.