Rais Samia aitega wizara ya kilimo kuhusu fedha alizotoa

0
41

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatavumilia kuona fedha za Watanzania alizotoa kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa kilimo zikichezewa.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja (Block Farms), utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji na kukabidhi mitambo na magari kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliyofanyika Chinangali, wilayani Chamwino.

“Sitavumilia pale nitakapotoa fedha za wavuja jasho wa Tanzania ziende kwenye matumizi ya kilimo na pesa ile ikachezewe, sitavumilia, nataka kuona kila shilingi itakayowekwa kwenye kilimo iende ikazalishe mara mbili au mara tatu,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali imejipangia kufikia mwaka 2030 mchango wa kilimo kwenye pato la taifa iwe asilimia 10 huku ikiendelea kutenga bajeti mahususi kwa ajili ya ajira mpya za watumishi wa sekta za umwagiliaji maji.

Aidha, katika ukuaji wa soko la bidhaa nje ya nchi, Rais Samia amebainisha kuwa bidhaa nyingi zinazozalishwa nchini hususani kwenye sekta ya kilimo zimekuwa zikipatikana sehemu nyingi duniani ikiwemo nchi za Ulaya.

“Ndugu zangu tunalisha dunia, hatuna maana kwamba dunia yote itasimama kuzalisha ilishwe na Tanzania hapana, lakini ukweli ni kwamba vitu vyetu [bidhaa] viko huko duniani, tunalisha dunia na tunataka tuendelee kulisha dunia,” ameeleza.

Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeazimia kutumia wilaya ya Makete kuwa sehemu maalum ya kuzalisha ngano ikiwa utafiti unaofanywa utakwenda sambasamba na matakwa ya Serikali.

“Wataalam kutoka Sokoine University, waalimu na wanafunzi wako wilaya ya Makete wanapima udongo wa Wilaya nzima [..] Mwenyezi Mungu akitujaalia na sayansi ikijibu kwamba ngano inakubali, tunaifunga wilaya ya Makete yote kwa ajili ya uzalishaji wa ngano,” amesema.

Send this to a friend