Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kufupisha safari yake ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) Dubai ili kurejea nchini kushughulikia kwa ukaribu janga la mafuriko lililokumba wilaya ya Hangang mkoani Manyara.
Mafuriko hayo ambayo yametokea Desemba 3, mwaka huu wilayani humo, yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 50 na wengine 80 wakijeruhiwa, huku idadi za kaya zilizoathirika ikiwa ni 1,150 na idadi ya watu walioathiriwa ni 5,600 ambapo pia takribani ekari 750 za mashamba zimeharibiwa.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali itagharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha kutokana na mafuriko hayo na kuelekeza majeruhi wote wanaohudumiwa katika hospitali mbalimbali kupatiwa matibabu yanayostahili kwa gharama za Serikali.
Rais pia ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wanapatiwa makazi ya muda, pia kufanyike tathimimi ya kina juu ya maafa hayo pamoja na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida.
Mbali na hayo, pia ametoa pole kwa wafiwa wote na kuwahakikishia kuwa Serikali inashughulikia masuala yote yaliyotokana na janga hilo.