Rais Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi kuacha tabia za kudharauliana wenyewe kwa wenyewe na kuwadharau wananchi, badala yake wakafanye kazi kwa misingi waliyoambiwa ili kuepuka migongano.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifunga mkutano wa faragha wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu na naibu makatibu uliofanyika kwa siku tatu jijini Arusha kuanzia Machi 02- 04, 2023 ambapo lengo kuu lilikuwa ni kuelekezana na kukumbushana kuhusu utekelezaji wa majuhukumu yao ili kuongeza tija na ufanisi wa utendaji wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
“Baada ya mafunzo haya na kama mlivyoazimia wenyewe twende tukaache migongano, twende tukaache kusengenyana, twende tukaaminiane tuache kuhujumiana, tuache uvivu, tuache uzembe ili tukafanye kazi za watu,” amesisitiza Rais Samia.
The Citizen yaamriwa kumlipa Mchechu fidia ya TZS bilioni 2
Ameongeza kuwa viongozi wa nyanja zote na katika nafasi mbalimbali wataweza kuleta mageuzi makubwa katika taifa endapo wataweza kubadili mitazamo yao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na kwamba mitazamo ya viongozi ikibadilika migongano na ubadhirifu katika maeneo ya kazi haitakuwepo kwani utendaji kazi utaimarika pia.
Aidha, Rais Samia amewaagiza viongozi kushirikiana na sekta binafsi ili kusaidia kuimarisha uchumi zaidi kwa kuvuta mitaji mikubwa, kuongeza ajira nchini, kukusanya kodi zaidi pamoja na kukuza biashara na uzalishaji.
Hata hivyo amewakumbusha viongozi kujiamini na kuwa tayari kusimama na kutetea maamuzi yao, kwani kwa kutojiamini hujiwekea vikwazo wao wenyewe.