Rais Samia akipa Chuo cha Diplomasia jina la Dkt. Salim

0
53

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Chuo cha Diplomasia kuanzia sasa kitafahamika kama Dkt. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa taifa hususani katika nyanja ya kidiplomasia.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa tovuti ya hifadhi ya nyaraka za Dkt. Salim Ahmed jijini Dar es Salaam ambapo amemwelezea Dkt. Salim aliyetumikia taifa akiwa kama Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Ulinzi na nafasi nyingine kuwa amehudumu nafasi hizo kwa uadilifu akiwa mchapakazi na mnyenyekevu kwa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

“Katika Nyanja ya kidiplomasia, Dkt. Salim aliwakilisha vyema taifa letu katika nchi na majukwaa mbalimbali ikiwemo Misri, India, China, Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Nchi huru za Kiafrika na kwingineko. Alijitahidi sana kuhusisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na taasisi alizohudumu,” amesema.

Balozi Amina: Sitagombea urais 2025, Rais Samia anatosha

Ameongeza, “Kwa sababu mcheza kwao hutunzwa na tumesema alikuwa mwanadiplomasia mahiri, tumekubaliana kukipa chuo kile cha Diplomasia jina, na sasa rasmi kitakuwa kinaitwa Dkt. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations.”

Aidha, Rais Samia amesema tovuti hiyo ni hazina kubwa kwa wanazuoni na watafiti wa masuala mbalimbali ya uongozi, ikifundisha viongozi na wanaotaka kushika nafasi za uongozi juu ya umuhimu wa uadilifu, uvumilivu, unyenyekevu na uzalendo, hivyo amewasihi viongozi kuiga kwa vitendo yale yote mazuri yaliyo katika tovuti hiyo.