Rais Samia akutana na bosi wa Barrick Gold, wazungumzia kampuni ya Twiga

0
43

Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Barrick Gold, Mark Bristow amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan Samia Barrick Gold itaendelea kushirikiana na Serikali katika Uwekezaji wa Sekta ya Madini nchini na wako tayari kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine. Amesema wanaendelea vizuri na mfumo wa utekelezaji wa makubaliano baina yao na Serikali katika kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika na rasilimali ya madini nchini.

Ametoa ahadi hiyo alipokutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dodoma na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi wa kampuni hiyo na kampuni ya Twiga.

Aidha, Bristow amesema kwa sasa Barrick imeajiri Watanzania wengi ikiwa ni pamoja na uongozi wa juu kama Mkurugenzi Mtendaji, Meneja Mkazi na Mkuu wa mahesabu kuwa ni Watanzania.

Ameongeza kuwa Barrick imefanya maboresho ya usimamizi wa mazingira katika Mgodi wa North Mara ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa kuhifadhi na kutibu maji yanayotokana na uzalishaji wa madini katika mgodi huo.

Ameongeza kuwa kwa sasa Barrick imeongeza ushiriki wa Watanzania katika kutoa huduma mbalimbali katika migodi yao ambapo takriban asilimia 70 ya manunuzi hutoka kwa Watanzania.

Kwa upande wake Samia amemhakikishia Muwekezaji huyo kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana nao kwa kutekeleza yale yote waliyokubaliana kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inanufaisha pande zote mbili kwa manufaa ya Taifa.

Aidha, Samia amemshukuru Bristow kwa utayari wake wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona nchini.

Send this to a friend