Rais Samia alivyodokeza mwisho wa bosi wa TPA

0
14

Rais Samia Suluhu Hassan mapema leo Julai 4 ametangua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi.

Uamuzi huo umekuja saa chache baada ya kueleza kuwa haridhishwi na mwenendo wa bandari nchini kutokana na kughubikwa na siasa na longolongo nyingi, mambo yanayoikosesha serikali mapato ambayo yangewezesha utekeleza wa shughuli za kijamii na maendeleo.

Maneno hayo yaliashiria mwisho wa bosi huyo ambaye amedumu kwenye nafasi hiyo tangu Aprili 2021 alipoteuliwa kuchukua nafasi ya Deusdedit Kakoko.

Akizungumza Ikulu leo amesema “Wale tuliowakabidhi uendeshaji wa bandari zetu wafanye kazi kwa kasi mno, siridhishwi kabisa na kasi za bandari, siasa zilizopo, longolongo zilizopo. Watu huko nje mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa. Sisi bado tunasua sua.”

Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) amesema utasaidia kuunganisha mikoa tisa ya Tanzania pamoja na kuunganisha Tanzania na nchi za jirani.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni mkoa wa Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Simiyu, Shinyanga na Mwanza. Pia nchi za jirani ikiwemo Uganda, Burundi, Rwanda, DRC na Sudan Kusini.

Hata hivyo, Rais Samia amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi kuifanyia kazi upya sheria ya PPP (National Public Private Partnership) na sheria ya manunuzi, kwa kuwa zimekuwa zikirudisha nyuma baadhi ya maendeleo.

Send this to a friend