Rais Samia alivyombana Askofu Gwajima hadharani chanjo ya Corona

0
25

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo amezungumza na wakazi wa Tegeta. Dar es Salaam na kuwaeleza masuala mbalimbali ambayo serikali inakusudia kuyafanya ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii (elimu, maji, afya, barabara).

Rais amezungumza na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani ambapo anaendelea kurekodi kipindi maalum cha The Royal Tour kinacholenga kutangaza utalii na fursa nyinginezo kutoka Tanzania.

Katika hali ambayo haikutarajiwa Rais Samia alimkaribisha mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima kuzungumza na wananchi, lakini kabla hajaanza, Rais alianza kuzungumza akiuliza kama wananchi watachanjwa ama la.

“Gwaji boy hoyeee. Tunachanja, hatuachanjiii? Tunachanja, hatuchanjiii?” aliuliza Rais Samia huku wananchi wakijibu kuwa watachanja.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake Gwajima hakugusia suala la chanjo badala yake alizungumzia matatizo mengine ikiwemo changamoto za upungufu wa madarasa kunakosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Hivi karibuni bunge limetoa adhabu ya kufungia mikutano miwili mbunge huyo kutokana na makosa mbalimbali likiwemo la kugonganisha mhimili wa bunge na mhimili wa serikali kupitia mahubiri yake kanisani ambayo amekuwa akishawishi wananchi kutochanjwa kwa madai kuwa chanjo si salama.

Alitiwa hatiani pia kwa kushusha hadhi na heshima za bunge pamoja na kuonesha dharau dhidi ya mhimili huo unaohusika kutunga sheria.

Send this to a friend