Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Prof. Abel Makubi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI) na kuchukua nafasi ya Dkt. Respicious Boniface ambaye amemaliza muda wake.
Pia, amemteua Omar Issa kuwa Mkuu (Chancellor) wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).
Issa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na anachukua nafasi ya Dkt. Gharib Bilali, Makamu wa Rais Mstaafu ambaye amemaliza muda wake.
Aidha, amemteua Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee kuwa Mkuu (Chancellor) wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Dkt. Mzee alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na anachukua nafasi ya Balozi, Dkt. Marten Y. C Lumbanga aliyemaliza muda wake.
Kadhalika, amemteua Dkt. Edwin Mhede kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB Plc kwa kipindi cha pili.