Rais Samia amuagiza Msajili wa Hazina kufuatilia hesabu za mashirika yote kwenye mfumo

0
64

Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kuhakikisha anaweza kuona hesabu za mashirika yote anayoyasimamia ikiwa ni pamoja na makusanyo na matumizi yao.

Ameyasema hayo katika hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika na Taasisi za Umma, iliyofanyika Juni 11, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo amesema ni muhimu kuona kile kinachoingia na kinachotoka kwani itasaidia kufahamu uwezo wa mashirika hayo kiuchumi na namna yatakavyoweza kujisimamia yenyewe.

“Yapo mashirika ambayo yanaweza kabisa kusimama yenyewe, mfano Ngorongoro inaweza kusimama yenyewe kwa sababu tumetengeneza mazingira watalii wanakuja mpaka wanacheua sasa kwanini isisimame, kwanini TANAPA isisimame yaani hakuna sababu.

Rais Samia asisitiza mashirika kuzalisha zaidi ili kuleta mageuzi ya kiuchumi

“Naziagiza bodi za mashirika kubadilika na kuyasimamia kikamilifu hakuna sababu ya mashirika na taasisi zote za Serikali katika kutekeleza hili. Hakuna sababu ya mashirika haya yasiweze kujisimamia yenyewe” amesema Rais.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema Ofisi yake ipo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti taarifa za kiutendaji na kwamba ofisi hiyo imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika vilivyoingizwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina.

Send this to a friend