Rais Samia aonya uzembe wa viongozi ubadhirifu wa fedha za umma

0
41

Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya viongozi wanaotumia vibaya fedha za halmashauri zinazotolewa na Serikali na kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha wanazuia na kupambana na vitendo hivyo.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tandahimba katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mfululizo wa ziara yake mkoani Mtwara inayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 19, 2023.

“Halmashauri hizi ziko chini ya Mkuu wa Wilaya, ziko chini ya viongozi kamati za siasa za Chama cha Mapinduzi, inakuwaje fedha inafika halmashauri inatumiwa vibaya inakuja kujulikana baadaye, na kwanini itumike vibaya? Madiwani mko wapi, kamati za siasa ziko wapi, wakuu wa wilaya wako wapi?” ameuliza.

Aidha, amesema Serikali inapotoa ruzuku inalenga kumtengenezea mazingira mazuri mkulima kwa kujenga uwezo wa kuzalisha mazao mengi zaidi ili Serikali iweze kupata mapato makubwa, hivyo amewaomba wananchi kufanya kazi na kuzalisha mazao mengi zaidi ya kiwango cha ruzuku kinachotolewa.

“Tunaleta ruzuku kuwajengea uwezo wa kuzalisha. Ruzuku shilingi moja ikazae shilingi tatu au shilingi tano, wewe ukafaidike na Serikali ikafaidike, haina maana kuleta ruzuku halafu mazao yanakuwa madogo,” ameeleza.

Mbali na hayo, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaacha watoto wa kike wasome kwa kuwa Serikali ilishaondoa gharama za elimu kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha sita.

Send this to a friend