Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema licha ya changamoto na hujuma zilizofanywa wakati wa kuanzisha kwa mradi huo, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alionesha umahiri na ukakamavu ili kutositisha mchakato huo.
Ameyasema hayo leo Desemba 22, 2022 wakati akitoa hotuba yake, mara baada ya kulifunga rasmi geti la handaki lililojengwa kuchepusha maji ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo lililopo Rufiji mkoani Pwani.
“Nakumbuka mikiki iliyokuwepo wakati ule, hujuma zilizofanywa wakati ule lakini kwa umahiri na ukakamavu marehemu alisema tunaendelea na tunafanya,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema mradi wa Bwawa wa Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) utasaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya Mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha uhakika cha umwagiliaji, kuimarisha fursa za kitalii katika eneo la kusini mwa Tanzania hasa hifadhi ya Taifa ya Nyerere pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.
Katika hotuba yake amebainisha kuwa Bwawa la Julius Nyerere ni miongoni mwa miradi mikubwa katika bara la Afrika hivyo Watanzania wana kila sababu ya kujivunia mradi huo ikiwemo kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata pale ikitokea mvua imepungua.
“Mradi huu unatoa ujumbe duniani kwamba Tanzania inaweza kutekeleza mambo makubwa ya kuweza kubadilisha hata taswira yake na ya ulimwengu,” ameeleza
Hapo awali Waziri wa Nishati, January Makamba amesema maji kwa kiwango kilichotathminiwa kimazingira yataendelea kupita na kuwanufaisha wakazi wa maeneo jirani hivyo wananchi waondoe taharuki.