Rais Samia apongezwa kwa kuimarisha amani, utulivu na maendeleo

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Twaha Ally Mpembenwe, amemsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi katika kuliletea Taifa maendeleo, huku akibainisha kuwa Serikali yake imeendelea kuimarisha amani, utulivu na mshikamano, misingi muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha mapendekezo ya nyongeza ya bajeti ya mwaka 2024/25, Mpembenwe amesema kuwa Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na sera na maamuzi ya Rais Samia.
Amesema Tanzania imeendelea kuwa kinara wa upatanishi wa migogoro barani Afrika, ikiwa ni sehemu ya falsafa ya Rais Samia ya 4R akitolea mfano namna Rais Samia alivyowapokea Wakuu wa Nchi za SADC na EAC ili kujadili suluhu ya mgogoro wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Aidha Mpembenwe ameeleza kuwa Rais Samia ametilia mkazo matumizi ya nishati safi, jambo lililoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika, ulioshirikisha marais 21 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Aidha, katika sekta ya utalii, Mpembenwe ameeleza kuwa juhudi za Rais Samia, ikiwa ni pamoja na filamu ya The Royal Tour, zimeongeza idadi ya watalii na kusaidia kupunguza nakisi ya Urari wa Jumla wa Malipo na Huduma kutoka Dola milioni 807.8 mwaka 2023 hadi Dola milioni 364.2 mwaka 2024.
Mpembenwe amesisitiza kuwa Kamati ya Bajeti itaendelea kuunga mkono sera za kiuchumi na kibajeti za Rais Samia, ili kuhakikisha Tanzania inazidi kusonga mbele katika maendeleo.
“Muda hautoshi kuelezea mafanikio ya Mheshimiwa Rais kwa kipindi ambacho amekuwa madarakani. Itoshe tu kusema anastahili kuendelea kuliongoza Taifa hili na tutarajie mengi mazuri zaidi chini ya uongozi wake,” amesema Mpembenwe.