Rais Samia apongezwa kwa kukuza biashara na uwekezaji

0
46

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo na ukiritimba uliokuwa unakwamisha ustawi wa sekta hiyo.

Dkt. Wanga amesisitiza kwamba sera mpya zilizotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia zimefungua uchumi wa nchi na kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma. Pia, Serikali imeanzisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya biashara.

Amesema TNBC chini ya uongozi wa Rais Samia, imeimarisha mabaraza ya biashara katika ngazi ya mikoa na wilaya, ambayo yamefanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara kushughulikia changamoto zao. Lengo la kuanzisha mabaraza haya ni kuhakikisha kwamba serikali za mitaa zinaweza kushughulikia masuala ya biashara na uwekezaji katika maeneo yao kwa urahisi.

Amebainisha kuwa kwa kuondoa ada na makato, Serikali imefanikiwa kupunguza gharama za biashara na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, na kusisitiza kuwa hatua hizo zimevutia uwekezaji mkubwa na makampuni yamefurahia faida na kuimarisha mtaji wao.

Aidha, amesema maboresho hayo ya mazingira ya biashara yameleta matumaini na fursa mpya kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini Tanzania, na yanatarajiwa kuchochea ukuaji na maendeleo katika sekta ya biashara na uwekezaji.

Send this to a friend