Rais Samia apongezwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Afrika

0
34

Rais Samia Suluhu Hassan amepongezwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa jitihada zake za kuendeleza ujasiriamali kwa wanawake na vijana nchini Tanzania.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa Mkutano wa 44 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa AU, unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo umepanga kujadili ajenda 15, ambapo ajenda sita tayari zimejadiliwa ikiwa ni pamoja na ajenda ya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama la AU ambapo Tanzania inaingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa nia ya kubakia kuwa mjumbe wa baraza hilo, ikichuana na nchi za Ethiopia, Uganda na Eritrea.

Kwa upande mwingine, wanawake wajasiriamali na vijana wanatazamiwa kunufaika na ajenda ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ukitarajiwa kuwawezesha kushiriki katika biashara za kimataifa zenye soko la zaidi ya watu bilioni 1.2 na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, Ajenda ya tatu ambayo Tanzania inaiamini ni ajenda ya elimu hususani kwa wasichana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu yatokanayo na vita, migogoro ya kisiasa na majanga ya asili.

Mkutano huo unafanyika kwa siku mbili, Februari 14 na 15 na utafuatiwa na Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali, utakaofanyika Februari 17 na 18, 2024 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan naye anatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.

Send this to a friend