Rais Samia aridhia msamaha wa riba kwa wadaiwa sugu kodi ya pango la ardhi

0
14

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kusamehewa riba ya kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa sugu kwa masharti kwamba wadaiwa hao wawe wamelipa madeni ya msingi ndani ya miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2022.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Nyachoka wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa zoezi la kukabidhi hati miliki za kimila.

Dkt Mabula alisema yeye pamoja na Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusamehe watakutana na kupanga namna bora ya kutekeleza msamaha huo.

“Najua kuna wengi wanadaiwa madeni ya muda mrefu kwa hiyo kumetokea msamaha kuanzia mwezi Julai mpaka Desemba mwaka huu, watakaoweza kulipa ndani ya miezi hii sita, wale ambao madeni yao yana miaka mitano kurudi nyuma watalipa bila ile tozo ya riba,” amesema Dkt. Mabula.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, mmiliki wa ardhi atakayeshindwa kulipa madeni yake katika kipindi cha miezi hiyo sita basi atadaiwa madeni yake pamoja na riba na akishindwa kufanya hivyo atafikishwa kwenye vyombo vya sheria ambako huko uamuzi wake ni kulipa ama kunyang’anywa ardhi anayoimiliki.

Akigeukia zoezi la utoaji hatimiliki za kimila Dkt Mabula alisema, hatua ya kumilikishwa ardhi kwa nyaraka kuna faida kubwa katika maisha ya kila siku na kutaja baadhi ya faida hizo kuwa ni pamoja na usalama wa ardhi, uhakika wa milki, kupunguza migogoro pamoja na nyaraka hiyo kutumika kama dhamana.

Send this to a friend