Rais Samia aridhia nyongeza ya mishahara kwa 23%

0
77

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia mapendekezo ya nyongeza ya mshahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa 23.3%.

Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa Ikulu ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichofanya hivi karibuni mkoani Dodoma na kupokea taarifa ya wataalamu kuhusu nyongeza ya mishahara.

Nyongeza hiyo imefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa katika mwaka 2022/2023 na hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi.

Kutokana na hatua hiyo katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi trilioni 9.7 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali.

Hivyo bajeti ya mishahara ya mwaka 2022/23 ina ongezeko la Shilingi trilioni 1.59 sawa na 19.51% ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22.

Wakati huo huo, Rais Samia amepokea mapendekezo ya kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni kama Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lilivyoomba Mei mosi, 2022.

Rais Samia ameridhia na kuielekeza wizara yenye dhamana na masuala ya hifadhi ya jamii kuendelea kushirikiana na TUCTA na Chama cha Waajiri nchini (ATE) ili kukamilisha taratibu za kuhakikisha malipo ya mkupuo ya 25% yaliokataliwa na wadau mwaka 2018 yanapandishwa hadi 33%.

Send this to a friend