Rais Samia Suluhu Hassan amesaini rasmi Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kuifanya kuwa sheria kamili na hivyo kufungua njia ya utoaji wa huduma za afya kwa kila Mtanzania.
Novemba 2 mwaka huu Bunge lilipitisha muswada huo kwa kishindo cha asilimia 100, tukio ambalo limeandika historia kufuatia kusimama kwa muda mrefu kwa kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2018.
Wizara ya Afya ilitoa taarifa ikithibitisha kwamba muswada huo umeshapata saini ya Rais na sasa ni sheria halali kwenye Gazeti la Serikali mnamo Desemba 1, 2023.
Hatua hii inatoa jukumu kwa Wizara ya Afya kuanza mchakato wa kutunga kanuni zitakazosimamia utekelezaji wa sheria hiyo ambayo inalenga kuondoa vizuizi vya kiuchumi na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya.