Rais Samia asema Afrika haitoendelea isipowekeza zaidi kwenye rasilimali watu

0
17

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni muhimu kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha wanaangalia, wanatathmini na kusimamia mageuzi yote muhimu ili kuliwezesha bara hilo kutumia uwezo na rasilimali zake kujikomboa kiuchumi.

Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu uliofanyika jijini Dar es Salaam, amesema bara la Afrika bado linahitaji mageuzi makubwa katika nyanja zote muhimu za uzalishaji na maendeleo, na kwamba idadi kubwa ya vijana iliyopo Afrika inaweza kutumika kama fursa ya kipekee kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi.

Aidha, Rais Samia amesema bara la Afrika halitajikomboa kiuchumi ikiwa nguvu kubwa haitaelekezwa kwenye maendeleo ya rasilimali watu kwa kutoa ujuzi na maarifa yanayohitajika.

Rais Samia: Tusiruhusu wenye nia ovu waligawe Taifa

“Hatuwezi kulikomboa bara letu kiuchumi kama hatutaelekeza nguvu zetu kwenye maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwapa maarifa na ujuzi unaohitajika katika kuyatumia na kuyabadilisha mazingira yao kwa manufaa yao,” amesema Rais Samia Suluhu.

Aidha, ametaja hatua mbalimbali ambazo Tanzania imechukua ili kukuza na kuendeleza rasilimali watu ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za lishe, huduma za afya ya uzazi wa mama na mtoto na kuanzisha vituo vya elimu ya awali nchi nzima.

Hatua nyingine ni uanzishwaji wa mfuko wa kusaidia kaya masikini (TASAF), programu ya elimu bila malipo kwenye ngazi za elimu ya awali, elimu ya msingi hadi sekondari, kuwezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri pamoja na kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kurudi tena shuleni.

Send this to a friend