Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kushangazwa na masoko kujengwa mbali na makazi ya wananchi, jambo alilotafsiri kwamba ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa wawakilishi wa wananchi katika utekeleza wa miradi hiyo.
Rais Samia amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), na kutaka wananchi washirikishwe kwenye miradi mbalimbali.
“Tumepita maeneo kadhaa katika ziara zetu, na unapopita unasikia malalamiko ya wananchi, kwamba soko limejengwa kule, sisi tuko huku. Kwa hiyo sisi kutoka huku kufuata soko kule inakuwa ni shida,” amesema Rais.
Amesema ukitizama hilo kwa undani unabaini kuwa mabaraza ya madiwani yamekaa na kujipangia bila kuwashirikisha wawakilishi wa wananchi, kwani wangeshirikishwa, makosa ya aina hiyo yasingetokea.
“Nimezunguka Dar es Salaam hapa, Temeke, masoko yamejengwa huko ambako hakuna watu. Sasa wanasema ‘ooh tutajenga vivutio vya watoto ili watu wavutike kuja, tutaweka route ya magari ili watu wavutike kuja,'” amesema Rais akisisitiza kuwa endapo upembuzi yakinifu ungefanyika vizuri soko lisingejengwa sehemu isiyo na watu kwani ingeonekana kuna dosari.
Ameagiza fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zitumike inavyopasa huku akigusia kibanda cha walinzi katika ofisi ya TANESCO kilichojengwa kwa zaidi ya TZS milioni 7, kwamba gharama yake ilitakiwa kuwa TZS milioni 3.
Serikali imepanga/imejenga masoko ya kisasa 22 nchini kote.