Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kushangazwa na vijana wa Tanzania kutokuwa na maadili licha ya kuwepo mifumo na taasisi nyingi ambazo zimejikita katika kutoa mafunzo ya kimaadili na kizalendo kwa watu tangu wakiwa na umri mdogo.
Ameeleza hayo wakati akihutumia mamia ya viongozi na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mlezi wa Skauti Tanzania mkoani Dodoma, ambapo amekitaka Chama cha Skauti Tanzania na taasisi nyinginezo kujiuliza swali hilo na kupata majibu.
“Lakini Tanzania tujiulize, ukiangalia mfumo wa Skuati, tuangalie mfumo wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umoja wa vijana wa vyama mbalimbali vya siasa, lakini tuangalie pia mfumo wa Girl Guides wetu. Tujiulize, ukosefu wa maadili, vitendo viovu vinatoka wapi Tanzania, tukiwa tuna taasisi zote hizi, zenye mifumo mikubwa ya kulea vijana, lakini bado tuna idadi kubwa ya vijana wanaopotoka,” amehoji Rais.
Akijibu ombi la chama hicho kutaka kuhamishiwa ndani ya Wizara ya Elimu amesema hilo hawezi kuahidi kwani akifanya hivyo vyama vingine navyo vitataka kurejeshwa wizarani, lakini atakachofanya ni kuhakikisha kuna kuwepo na mfumo wa kuiwezesha Skauti kufanya shughuli zake.
Amesisitiza chama hicho kuendelea kutoa mafunzo kwa watoto, ili kujenga viongozi wa baadaye waliowazalendo akibainisha kwamba “Nakshi ukichora kwenye jiwe, hazifutiki maisha. Lakini ukichora kwenye mchanga zinafutika. Kwa hiyo, mtoto mdogo amefananishwa na jiwe linalochorwa ile nakshi.”
Ameahidi kuwa katika uongozi wake kama Rais na Mlezi wa Skauti atahakikisha kinaimarika zaidi na kufikia lengo la kuwa na wananchama milioni 4 ifikapo mawaka 2023, kutoka wanachama 800,000 wa sasa.