Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya msaada wa shilingi bilioni 455.09 kwa ajili ya utekelezaji wa programu tatu za maendeleo, na msaada wa shilingi bilioni 117.04 kwa ajili ya bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2022/23 kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Hafla hiyo ya utiaji Saini imefanyika leo Julai 04, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwa ni katika mwendelezo wa mpango mkakati wa miaka saba wa kusaidia serikali ya Tanzania ulioanza mwaka 2021.
Aidha, mikataba mitatu kwa ajili ya utekelezaji wa programu tatu za maendeleo ni Uchumi wa Buluu wenye thamani shilingi bilioni 279.20, mkataba wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za serikali na kukuza sekta binafsi wenye thamani ya shilingi bilioni 160.79.
Mkataba wa tatu uliosainiwa ni wa kuimarisha mahusiano kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania ili kuongeza ufanisi katika kubuni na kusimamia miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya wenye thamani ya shilingi bilioni 15.23.
Rostam aomba radhi kwa kauli yake dhidi ya Mahakama
Akizungumza Rais Samia Suluhu katika hotuba yake amesema kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kumeimarisha biashara pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka Umoja huo, ambapo kwa mwaka 2022 idadi ya watalii ilifika 449,200 kutoka watalii 362,393 mwaka 2019.
Naye mwakilishi na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Manfredo Fanti amesema wanategemea mchango unaotolewa na umoja huo kupitia mikataba hiyo utaleta chachu katika maeneo yenye kubeba fursa za kukua katika ubunifu pamoja na kupongeza juhudi za Rais Samia Suluhu katika mabadiliko ya kisera yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia.