
Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa Mahakama hususan Mahakama za Mwanzo kutokufungwa na masharti ya kiufundi katika utoaji haki ili kurahisisha upatikanaji wa haki na kuzidi kujenga imani kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo Aprili 05, 2025, wakati wa uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania uliofanyika katika eneo la Tambukareli, jijini Dodoma.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa jengo hilo lililogharimu shilingi bilioni 129.7 kutunzwa na kutumika ipasavyo huku akisisitiza uwekezaji uliofanywa uendane na ubora wa huduma kwa wananchi.
“Serikali imefanya makusudi kujenga mazingira mazuri kwa majaji wetu. Lakini mazingira haya yaendane na huduma bora zinazotolewa ndani ya majengo haya,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesisitiza haja ya Mahakama ya Tanzania kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma za kimahakama ili kuendana na kasi ya dunia pamoja na kurahisisha uendeshaji wa mashauri na upatikanaji haki.