Rais Samia asisitiza ushirikishwaji Sekta binafsi katika utoaji huduma za afya

0
15

Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika kongamano la pili la kumuenzi aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, lililofanyika visiwani Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema kupitia kumbukizi hiyo, inakumbusha wajibu na umuhimu wa ushupavu wa uongozi katika kuyafikia mabadiliko.

Vigogo 39 wadaiwa kukwepua eneo la wananchi Mwanza, Waziri aingilia kati

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzishirikisha Sekta binafsi na kuziamini katika kutoa huduma za afya kwa wananchi, ili Tanzania iende kwa kasi na kupata matokeo inayoyataka.

“Nilishapokea maombi Sekta binafsi wanataka kufunga, kuweka mitambo ya vipimo vya afya katika maeneo kadhaa Tanzania, hakuna anayewasikiliza wala hawakaribishwi kuambiwa basi karibuni, mkakati unasema hivi, njooni tupange tunafanya vipi,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa ni vema kujitathmini hatua gani zimepigwa katika ushirikishwaji na kuweka mazingira mazuri kwa Sekta binafsi kushiriki kwenye ubia na Serikali katika utoaji wa huduma bora za kiafya.

Amesema, kupitia mikakati na miongozo ya kitaifa na kisekta, Serikali imebainisha umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu katika sekta ya afya kwenye jamii pamoja na vituoni.

Rais Samia ametoa wito kwa wasimamizi wa masuala ya rasilimali watu kwenye sekta ya afya kutoa kipaumbele zaidi kuharakisha utekelezaji wa mikakati ambayo tayari imebainishwa ili kutatua changamoto za watumishi.