Rais Samia ataja sababu ya watalii kukaa nchini siku chache

0
66

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa moja ya sababu zinazofanya watalii kukaa siku chache nchini ni wigo mdogo wa shughuli za utalii ambazo zimejikita zaidi kwenye utalii wa maliasili, wanyamapori, fukwe na milima.

Rais amesema hayo leo mkoani Mwanza wakati akizungumza katika Tamasha la Utamaduni lililoandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania na kusema pamoja na kuwa utamaduni hutangaza mila na desturi za nchi lakini pia ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwa sababu ni moja ya vivutio vya utalii.

“Nimewahi kusikia kuwa moja ya mambo yanayofanya nchi yetu ipokee idadi ndogo ya watalii, na watalii wengine wanaokuja kutokurudi tena nchini ni kuwepo kwa wigo mdogo wa shughuli za kitalii,” amesema Rais Samia.

Amesema serikali imejipanga kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ukiwemo utalii wa utamaduni ambapo tayari ameanza kuchukua hatua za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii, biashara na uwekezaji nchini kupitia filamu inayoendelea kurekodiwa na Kipindi maarufu cha Royal Tour.

Sekta ya utalii huchangia wastani wa asilimia 17 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira takribani milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka. Aidha, sekta hiyo huchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda, biashara, kilimo, mifugo na usafirishaji.

Send this to a friend