Rais Samia ataka nyumba za ibada zitumike kuimarisha amani

0
62

Rais Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kujenga Taifa la watu wenye hofu ya Mungu, heshima, upendo, maadili mema na itikadi ya kudumisha amani na utulivu.

Ameyasema hayo leo mjini Bukoba mkoani Kagera wakati akifungua msikiti wa Jami`ul Istiqama Bukoba.

“Tukiendeleza kuzienzi tunu zetu hizi, basi bila shaka amani katika nchi yetu itaendelea kudumu, tukumbuke kuwa neema hii ya amani tuliyonayo inatamaniwa na nchi nyingi duniani, hivyo tuilinde kwa juhudi zetu zote kama ni dua au sala tulinde amani yetu,” amesema.

Aidha, mesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini kwa karibu zaidi kuhakikisha miradi na mipango ya maendeleo ya kijamii na kiimani yenye kuleta manufaa inatimia.

Mbali na hayo, amewaasa viongozi kuepusha mikwaruzano kwa kutaka madaraka pindi nyumba za ibada zinapojengwa kwa kujali zaidi maslahi yao binafsi.

“Katika maeneo mengine kuna zuka mifarakano kunapojengwa misikiti kama hii. Nimeona msikiti huu una maduka, mifarakano huja kwenye kutaka madaraka ya kusimamia na kuendesha msikiti huu hasa kunapokuwa na biashara zinazoleta riziki, biashara inayofanywa hapa itoe sadaka ndogo ya kuendeleza msikiti huu,” amewaasa.

Baada ya ufunguzi wa msikiti huo Rais Samia amehitimisha rasmi ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera na kurejea jijini Dododma kwa ajili ya shughuli za kiserikali.

Send this to a friend