Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazocheleweasha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika leo Februari 1, 2023 jijini Dodoma, Rais Samia amewataka majaji na mahakimu pamoja na wadau wote katika sekta ya sheria kupitia upya taratibu ambazo mashauri hupitia ili kuzifupisha kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa haki unafanywa kwa haraka na kuepusha migogoro mbalimbali kwenye jamii.
“Nchi yetu imejengwa kwa misingi inayozingitia haki, inayodumisha amani na ambayo inaweza kuwepo au kupotea endapo migogoro inayofikishwa mahakamani haitatuliwi kwa haraka” amesema.
Rais Samia aagiza taasisi tano kuchungwa
Aidha, akieleza jitihada za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa haki, Rais Samia ameelekeza pesa zilizotoka katika Benki ya Dunia kuimarisha miundombinu ya mahakama za mwanzo 60, majengo 18 ambapo kati ya majengo hayo 11 ni mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo saba.
“Serikali itaendelea kushirikiana na mahakama kwa kuwezesha miradi hiyo ili kuweka mazingira wezeshi ya kufanya kazi na kusaidia wananchi kupunguza gharama katika kutafuta haki,” ameeleza.