Rais Samia ateuliwa kuwa mjumbe wa masuala mabadiliko ya tabianchi duniani

0
74

Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation – GCA).

Taarifa ya uteuzi huo imewasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, wakati alipokutana na Rais Samia pembezoni mwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi jijini Nairobi, Kenya.

“Heshima hii ni utambuzi wa uongozi mahiri wa Rais Samia katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi Afrika na duniani kote, ambapo Tanzania ni kinara kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali barani Afrika,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari.

Aidha, Wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Rais wa Senegal, Macky Sall, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Mahmat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinumwi Adesina, na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.

GCA ni taasisi kubwa duniani inayosimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, na hadi sasa imeweza kufanikisha upatikanaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 50, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi za kwanza zitakazonufaika na fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Send this to a friend