
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Shilingi bilioni 5.2 kwa Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya kuboresha Chuo cha Kikanda cha Mafunzo ya Uhamiaji (TRITA) kilichopo mkoani Kilimanjaro. Amesema juhudi hizo zinalenga kukipanua chuo hicho ili kuanza kutoa elimu katika ngazi ya Shahada, Uzamili na Uzamivu, huku kwa sasa kikitoa mafunzo ya ngazi ya Diploma.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Najma Murtaza Giga, kwa lengo la kukagua miradi iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
“Ni chuo ambacho kimejikita zaidi kwenye taaluma ya soft skills(ujuzi laini) ila mafunzo ya medani yanatolewa Chuo cha Raphael Kubaga kilichopo Wilayani Mkinga, mkoani Tanga kwa hapa tunakusudia kama tutafanya vizuri zaidi na kwa kuwa Mheshimiwa Rais anaviwezesha vyombo vilivyopo chini ya wizara kifedha basi tuna matumaini ya kufika kwenye hatua ya kutoa elimu ngazi ya Shahada, Uzamili na Uzamivu inawezekana kwa eneo hili ukiwepo urahisi wa kufika na tunapata wanafunzi kutoka nchi za jirani” amesema Waziri Katambi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Anna Makakala, amesema Idara hiyo sasa imeanza kutoa mafunzo ya kijeshi katika chuo cha Mkinga, badala ya kutegemea vyuo vya taasisi nyingine kama vile Polisi, Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Najma Giga, amesisitiza umuhimu wa Idara ya Uhamiaji kuwekeza zaidi katika mifumo ya teknolojia ili kuongeza ufanisi wa utendaji katika maeneo mbalimbali.
Aidha, mjumbe wa kamati hiyo, Nape Nnauye, amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa elimu kwa njia ya masafa ili kupanua fursa za mafunzo kwa wanafunzi wengi zaidi.









