Rais Samia atoa Bilioni 511 kulipa madeni ya makandarasi

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema katika kipindi cha siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan wamepokea jumla ya shilingi Bilioni 511 kwaajili ya kulipa madeni ya makandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Ulega amesema kati ya fedha hizo bilioni 280 zimetoka hazina na zilizosalia zimetoka katika miradi ya wafadhili wa miradi ya ujenzi.
“Kati ya hizi Bilioni 280 za hazina, Bilioni 125, zimetoka kwenye mfuko wa barabara na zimelipa wakandarasi wadogo wazawa wanaotekeleza miradi ya ujenzi,” amesema Waziri Ulega.
Katika hatua nyingine, Ulega amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kufanya maboresho ya kimuundo na kiutawala kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ili kuongeza ufanisi na udhibiti wa fedha za umma suala ambalo liliifanya TEMESA kushindwa kulipa madeni.
Waziri Ulega amesema kwasasa wamechukua hatua zaidi za kuboresha Uongozi wa wakala huo, akisisitiza kuwa kuwapo kwa usimamizi na mifumo sahihi katika wakala huo, kutawezesha ulipaji wa madeni yanayodaiwa kwa wakala huo, akisema uongozi uliokuwepo ulisababisha pia ubadhirifu wa fedha kutokana na kuwa na watu wasiokuwa waaminifu.









