Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanadiplomasia Namba Moja, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka mabalozi wa Tanzania kutilia maanani na kutekeleza yale yote wanayoyajadili na kukubaliana katika kikao kazi cha mabalozi kinachoendelea katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Ameongeza kuwa utekelezaji huo si tu wa makubaliano yatakayofikiwa mwaka huu, bali pia utekelezwaji wa yale yaliyoafikiwa katika kikao kazi cha mabalozi kilichopita pamoja na utekelezwaji wa diplomasia ya umma kwa haraka.
Akizungumza na mabalozi hao kwa njia ya mtandao, Rais Samia amewataka mabalozi kulinda maslahi ya kiuchumi na madini ya watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazoendelea nyumbani (Tanzania).
“Ni vizuri kufuatilia kwa ukaribu yanayoendelea nyumbani na kama kuna suala la ufafanuzi msisite kutoa ufafanuzi,” ameelekeza Rais Samia.
Rais Samia amewataka mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao kutilia maanani kukuza utalii, uchumi wa buluu na uvivu, maeneo ambayo ndiyo vyanzo vikubwa vya uchumi Zanzibar.
Aidha, amewasihi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu, bidii na maarifa.