Rais Samia atoa onyo kwa wezi wa vifaa miradi ya maendeleo

0
31

Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya Watanzania wasio waaminifu wanaoiba vifaa katika miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini.

Ameyasema hayo jana Juni 14, 2023 mkoani Mwanza wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja la JPM (Kigogo-Busisi) pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza (Hapa Kazi Tu).

“Wanaoiba saruji na vifaa vingine vya ujenzi waache mara moja kwa sababu miradi hii ni yetu sote, kukamilika kwao ni faida kwetu sote,” amesema Rais Samia wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

CHADEMA yatangaza kutoshiriki uchaguzi wa madiwani

Onyo hilo limefuatia baada ya wizi wa mara kwa mara kuripotiwa katika miradi mikubwa ikiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na daraja la JPM ambapo matukio ya wizi wa saruji, mafuta na vifaa vingine vya ujenzi yamefanyika.

Aidha, akisoma taarifa ya hali ya ujenzi wa daraja la JPM, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mohamed Besta, amesema utekelezaji wa mradi huo tayari umefikia asilimia 75, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo UVIKO-19, kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Victoria, na tofauti za hali ya kijiolojia ambayo ilichelewesha utekelezaji wake kwa asilimia 14.

Send this to a friend