Rais Samia atoa rai kwa viongozi kuiga mfano wa Sokoine

0
53

Rais Samia Suluhu ametoa rai kwa viongozi kuiga sifa za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine katika uongozi ikiwa ni pamoja na uadilifu na uchapakazi pasipo kuweka mbele maslahi binafsi.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kitabu cha Edward Moringe Sokoine katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, amesema kiongozi huyo alikuwa mwajibikaji, mzalendo pamoja na mwaminifu katika nafasi yake, hivyo akapata nafasi ya kuaminiwa kwa kupewa nafasi ya Waziri Mkuu akiwa katika umri mdogo.

“Sokoine alikuwa mwaminifu sana kwa mamlaka yake ya uteuzi na kwa wananchi, ndio maana haishangazi kwamba alikasimiwa majukumu mengi na makubwa ikiwemo uwaziri mkuu katika umri mdogo. Ukiwa mwadilifu na mchapakazi huna haja ya kukimbizana na vyeo bali vyeo vitakufuata ulipo,” ameeleza.

Aidha, amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 34 kwa ajili ya mradi wa makumbusho ya marais ambao utajengwa jijini Dodoma ili kuweka historia na kumbukumbu za viongozi hao walioacha alama.

“Nataka nitoe taarifa kwamba pendekezo hili limeanza kufanyiwa kazi, kuna mradi wa makumbusho ya marais, mradi huu ni mradi namba 5221 eneo liko Mtumba na tumetenga TZS bilioni 34 kwa ajili ya mradi huu na mwaka huu tumeanza kutenga bajeti ndogo kama bilioni 1 na kitu na eneo lile lina ukubwa wa ekari 50 pale Dodoma kwahiyo hili tunalifanyia kazi,” amesema.

Mbali na hayo, amewataka viongozi kutojisahau katika kusimamia nidhamu ya watoto wao kama ambavyo Sokoine alivyohakikisha anasimamia malezi ya watoto wake hata pale alipokasimiwa majukumu mengi ya kiserikali.

Send this to a friend