Rais Samia atunukiwa tuzo maalum na wakandarasi nchini

Rais Samia Suluhu amepewa tuzo maalumu na wakandarasi nchini kwa kuthamini mchango wake na hatua alizochukua kwenye sekta ya ujenzi tangu aingie madarakani.
Tuzo hiyo imepokelewa kwa niaba yake na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, katika tukio lililofanyika ukumbi wa The Super Dome, Dar es Salaam.
Akizungumza katika tukio hilo, waziri Ulega amesema uamuzi wa kumpa tuzo Rais Samia ni stahiki kwa sababu mambo ambayo ameyafanya kwenye uongozi wake yanaonekana.
“Wakati mwingine sisi ambao tunaishi Tanzania hatuoni au tunaweza kubeza kile kilichofanyika. Lakini juzi hapa, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, amesema siku hizi anapotea akija Dar es Salaam kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya kimiundombinu yanayoendelea,” amesema.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Wakandarasi na Miundombinu (CCIZ), Steven Mkomwa, amesema sekta hiyo imepata maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni ingawa kuna changamoto zinahitaji kufanyiwa kazi.








