Rais Samia aunda timu ya kuandaa mkakati wa kuwainua wanawake

0
38

Rais Samia Suluhu Hassan ameunda timu ya wataalamu ambayo inaangalia namna bora kwa Tanzania kufanikiwa katika kupata usawa wa kijinsia wakati wa uongozi wake, na timu hiyo itatoa mapendekezo kadhaa ya kuwainua wanawake katika vita dhidi ya umasikini. 

Amesema hayo aliposhiriki Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali Wanawake wanaoshiriki mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Marekani na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia licha ya vikwazo vinavyojitokeza.

Ameeleza kuwa tangu amekuwa Rais ameendelea kuteua viongozi wanawake katika nafasi mbalimbali ambazo hazijawahi kushikwa na wanawake ili kuondokana na dhana ya kuwa kuna nafasi ambazo wanawake hawawezi.

“Hivi karibuni nimemteua Waziri wa Ulinzi ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo nchini mwetu, ili kuondokana na dhana kuwa wanawake wanaweza nafasi fulani tu,” amesema Rais Samia.

Maeneo ambayo timu hiyo inapitia ni pamoja na marekebisho ya sheria kandamizi, sera na mikakati ya kuwasaidia wanawake katika kupata fursa kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ajira, elimu na nyinginezo za kuwainua kiuchumi kama vile kumiliki ardhi, kupata mikopo na nafasi za uongozi.

Send this to a friend