Rais Samia awaasa wananchi kulinda amani ili kuvutia uwekezaji 

0
45

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuitunza amani na utulivu uliopo na endapo kunatokea tofauti yoyote ni vyema kujadili ili kupata suluhu itakayokuwa na manufaa katika kudumisha nchi.

Ameyasema hayo leo kwenye kongamano la Wanawake wa Kiislamu Zanzibar Mwezi 27 katika maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 – Hijiria mjini Zanzibar.

“Nilikuwa namsikiliza Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania anahojiwa akasema mwezi Mei na Juni tumepokea wawekezaji kiasi ambacho hatujawahi kupokea, lakini ukitazama sababu ni kwamba kwa jirani kunawaka moto na mwekezaji hakai kunakowaka moto wanakimbia wanakuja zao kwenye amani na utulivu,” amesema.

Aidha, Rais Samia amesema udhalilishaji wa kijinsia unadumisha na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwakuwa wanawake wana uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa kuanzia katika ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.

“Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki, kushiriki katika mambo ya kitaifa na jamii kwa kufanya mambo na kazi ambazo huko nyuma zilionekana si za mwanamke kwa kudhaniwa kuwa hawezi kuzifanya, lakini leo tunazifanya kwa uhakika na weledi mkubwa,” ameeleza.

Mbali na hayo, ameisihi jamii kuiga mifano mizuri na inayooneshwa na viongozi wa dini hasa katika kutumia njia bora na hekima katika kuendesha maisha ya kila mmoja.

Send this to a friend