Rais Samia awajibu wanaohoji kuhusu Machifu

0
42

Akizungumza katika Tamasha la Utamaduni mkoani Kilimanjaro, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inashirikiana na machifu na wazee wa kimila mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuenzi na kutunza utamaduni na maeneo yaliyotuzwa.

“Tumeamua kuwa na jukwaa la pamoja baina ya serikali, machifu na wazee wa kimila ili tushirikiane katika kuhifadhi mila na desturi zetu, na katika kuhifadhi maeneo mbalimbali yaliyotunzwa, kama njia ya kuhifadhi mazingira ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Majibu hayo ya Rais yamekuja kufuatia kuwepo mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya wachangiaji walikuwa wakihoji kuhusu serikali kudumisha masuala ya kichifu ambayo kwa mujibu wao yalifutwa mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru ili kudumusha umoja wa kitaifa.

Licha ya umuhimu huo, Rais Samia amesema utamaduni ndio utambulisho wa Taifa na kwamba mataifa mengine yamekuwa yakifanya vizuri kwa kufanikiwa kuuonesha utamaduni wao kiasi cha kufikiwa kuigwa na watu wengine kwenye mataifa mengine.

“Utamaduni ni utambulishoi wa Taifa, ni ajira, ni kivutio cha utalii na ni uchumi pia. Nchi huheshimika kutokana na utamaduni wake. Ni wakati sasa wa kuzionesha tamaduni zetu zote nzuri ili dunia iweze kuzijua na kuja kuziona,” ameisisitiza.

Amewataka viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa kufanya matamasha hayo na kuwarithisha vijana utamaduni wa Tanzania ili usisahaulike.

Pia ametumia jukwaa hilo kuwapa pole wananchi wote waliopoteza mifugo yao iliyokufa kutokana na ukame uliokumba maeneo yao.

Amewataka wafugaji kushirikiana na Serikali ili kutumia mafunzo waliyoyapata kutokana na janga la ukame kuona namna bora ya kuanza ufugaji wa kisasa usiotegemea mvua katika kupata malisho.

Send this to a friend