Rais Samia: Awamu ya tano ilikuzwa heshima ya woga

0
34

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuondoa heshima ya woga ambayo ilijengwa katika awamu ya tano na badala yake wajenge heshima kutoka mioyoni mwao.

Ameyasema hayo leo Aprili 2 wakati akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo amewaasihi kujenga heshima ya kweli, kuheshimiana na kuacha migogoro kati ya viongozi Serikalini.

“Heshima iliyokuzwa ni heshima ya woga kwa sababu kulikuwa na Simba wa Yuda ambaye alikuwa ukimgusa sharubu anakurarua. Heshima inayotakiwa iwe ya moyoni, kila mmoja awe na itikadi moyoni mwake kwamba mimi ni mtumishi wa serikali majukumu yangu ni haya, line yangu ni hii sitakiwi kuvuka huku,” amesema.

Aidha ameeleza kuwa, kwa upande wa Serikali inakwenda kufanya maboresho katika Chuo cha Utumishi wa Umma na Chuo cha Uongozi kwa ajili ya kuwapa watumishi wa umma mafunzo, hivyo Baraza la Maadili likisimama kwenye sheria na kurekebisha maadili ya watenda kazi wa Tanzania, nchi itakwenda vizuri.

Rais Samia amewasihi kutokuendekeza nafsi na kufanya kazi kwa kufuata mipango, sheria, miongozo, pamoja na Dira ya Maendeleo ya nchi ili kukuza ustawi wa taifa.

Katika hafla hiyo Rais Samia amesema hayo leo mara baada ya kuwaapisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili pamoja na Wajumbe wake wawili na viongozi wengine pia katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.

Send this to a friend