Shirikisho la Umoja wa Machinga wilayani Kahama mkoani Shinyanga limekabidhiwa kiwanja chenye hatimiliki pamoja na TZS milioni 10 ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa ofisi yao.
Akizungumza Katibu Mkuu wa shirika hilo, Venatus Magayane amesema kila Mkoa wenye wafanyabiashara hao, Rais Samia amewapa TZS milioni 10 na kiwanja chenye hatimiliki kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, hivyo baada ya ujenzi kukamilika machinga watakuwa na nafasi ya kukopesheka na tassisi za kifedha tofauti na hapo awali.
Amesema kwa sasa wameridhishwa na lengo la Serikali chini ya Rais Samia katika kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira rafiki.
Mmoja wa Machinga, Agnes Magoli amesema mara ofisi zitakapokamilika zitawasaidia kuwa wafanyabiashara wakubwa ambao watakuwa wakichangia kodi Serikalini kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Aidha, kwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia kwa Machinga hao, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amewaongezea TZS milioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi hiyo.