Rais Samia awapongeza Watanzania walioshinda medali nchini Uswisi
Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza vijana wa Kitanzania walioibuka washindi wa pili na kupata medali ya fedha katika mashindano ya kwanza ya Global Robotics Challenge yaliyofanyika Geneva Uswisi yaliyoshirikisha mataifa zaidi ya 190.
Rais Samia amefarijika kusikia kuwa roboti iliyoundwa na vijana hao chini ya maudhui ya kukamata hewa ukaa (Carbon dioxide) inaweza kusaidia kusafisha kaboni hewani na kusaidia kupunguza ongezeko la joto kwenye angahewa ya Dunia.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 15, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia katika hafla ya kuwapongeza vijana hao iliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Nitumie nafasi hii kuwaahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kufuatilia maendeleo yenu na kuona namna ya kuendeleza vipaji vyenu. ” amesema.
Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuandaa mpango wa kuwa na vituo vya ubunifu nchini katika ngazi za mikoa na wilaya mbalimbali ili kusaidia kuinua vipaji vya vijana.
Amesema Wizara iimarishe utaratibu wa kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu mbalimbali ili kuwapa motisha na kukuza ajira nchini na pia ishirikiane na mamlaka husika kuandaa utaratibu wa kuwasaidia wabunifu mbalimbali na kuwaunganisha na taasisi pamoja na makampuni kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wa kazi zao kulingana na mahitaji.