Rais Samia awasha umeme wa gridi ya Taifa na kuzima jenereta la Kasulu
Rais Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 17, 2022 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi amewasha umeme wa Gridi ya Taifa katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kuzima mitambo mitatu ya mafuta yenye uwezo wa kuzalisha megawati 3.75 za umeme na kusambaza kwenye maeneo ya Wilaya ya Kasulu na Buhigwe.
Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia mitambo hiyo, maeneo ya Wilaya za Kasulu na Buhigwe yalikuwa yakipata umeme wa megawati 3.75 ambao haukutosheleza mahitaji na hivyo wananchi kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi na uwekezaji.
Imeeleza kuwa Serikali kupitia TANESCO ilikuwa ikitumia gharama kubwa za mafuta za TZS bilioni 13 kwa mwaka na matengenezo ya mitambo za TZS bilioni 1 kwa mwaka wakati wa makusanyo kwa wilaya zote za Kasulu na Bahigwe ni TZS milioni 364 tu.
TANESCO imesema kwa sasa Wilaya za Kasulu na Buhigwe tayari zimeunganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa kutoka kwenye kituo kikubwa cha Nyakanazi kupitia Wilaya za Kakonko na Kibondo na hivyo kuondoa kabisa gharama kubwa za uendeshaji mitambo pamoja na uhaba wa umeme uliokuwepo na kusaidia shughuli za uchumi na uwekezaji.