Rais Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa majaji na mahakimu wote nchini kuwajibika kwa kufanya kazi zao kwa uadilifu na kutenda haki, kwani kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu.
Ameyasema hayo wakati akishiriki maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma ambapo amewataka majaji na mahakimu kufuata Ibara ya 107A(2) ya katiba ambayo inaelekeza kutenda haki, kutochelewesha haki bila sababu za msingi, kutofungwa na masharti ya kiufundi kupita kiasi na kutoa kipaumbele katika usuluhishi.
“Mimi naamini ukitoa hukumu kwa dhuluma unajua kabisa kwenye nafsi yako kwamba umedhulumu haki ya mtu au haki ya jamii, alisema mmoja wetu hapa, kwamba maandiko matakatifu yanatuambia dhambi ni aibu kwa jamii na ukitoa hukumu ya dhuluma umetenda dhaki na unaipelekea jamii aibu,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali imeendelea kushirikiana na mahakama kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili mahakama ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa maarufu kama vituo jumuishi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kufanya uwekezaji kwenye TEHAMA.
Mbali na hayo ameigiza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau kutekeleza kikamilifu mfumo wa utoaji wa msaada wa kisheria kwa mujibu wa sheria zilivyo.