Rais Samia Suluhu Hassan amesema wachimbaji wa madini watakaouza dhahabu zao katika viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyoko nchini watapata punguzo la asilimia 3 ya tozo za serikali kwenye mauzo ghafi ya madini yao.
Ameyasema hayo Oktoba 21, 2023 wakati wa akizundua vifaa mbalimbali vya uchimbaji madini kwaa jili ya kuimarisha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na wachimbaji wadogo mkoani Dodoma ambapo mitambo mitano ya uchorongaji wa madini yenye thamani ya TZS billioni 2.73 pamoja na mitambo 10 ya kuponda mawe itakayofanya kazi katika maeneo ya wachimbaji wadogo imezinduliwa.
“Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuboresha shughhuli za uchimbaji mdogo ikiwemo kufuta kodi ya ongezeko la thamani ya asilimia 18 pamoja na kodi ya zuio ya asilimia 5 kwa wachimbaji wadogo watakaouza madini yao kwenye masoko ya madini ya hapa ndani,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema STAMICO imeweza kutafsiri kwa vitendo dhana ya mageuzi ambayo Serikali inayatekeleza, na kutoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo, huku akitoa rai kwa wadau kuendelea kuliamini shirika hilo na kushirikiana kibiashara kutokana na ubunifu, umakini na ueledi wa shirika hilo kuleta tija kwa taifa.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa shughuli za uchimbaji mdogo katika kutoa ajira, kuboresha kipato cha mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla, na kwamba sekta hiyo inakwenda kuwa sekta muhimu katika ukuaji wa nchi pamoja na kustawisha maisha ya wachimbaji wadogo.